Kristoforo Kolumbus

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Kristoforo Kolumbus
Jahazi ya Santa Maria imejengwa tena kwa mfano wa jahazi ya Kolumbus miaka 500 iliyopita
Msanii alichora picha hii mwaka 1893 akitaka kumwonyesha Kolumbus jinsi alivyofika Amerika mwaka 1492

Kristoforo Kolumbus (Kiitalia: Cristoforo Colombo, Kihispania: Cristóbal Colón, Kilat.: Columbus, * 1451 Genova; † 20 Mei 1506 Valladolid) alikuwa mfanyabiashara na mpelelezi aliyegundua njia ya usafiri kati ya Hispania na Amerika.

Mara nyingi aliitwa Mzungu wa kwanza wa kufika Amerika lakini baadaye imejulikana ya kwamba Waviking walitangulia kufika Amerika ya Kaskazini mnamo mwaka 1000. Lakini jitihada zake zilianzisha njia ya mawasiliano ya kudumu kati ya Amerika na mabara mengine tofauti na safari zote zilizovuka bahari kabla yake.

Kolumbus alizaliwa Italia mwaka 1451 akafa 20 Mei 1506. JIna lake la Kiitalia lilikuwa Cristoforo Colombo; Kihispania aliitwa Cristóbal Colón.

Mipango ya Kolumbus[hariri | hariri chanzo]

Nia ya Kolumbus ilikuwa kugundua njia ya kufika Uhindi kwa kuelekea magharibi. Sababu yake ilikuwa hali ya siasa wa wakati wake: njia zote za mawasiliano kati ya Ulaya na Uhindi zilitawaliwa na Waislamu. Bei za mali zote zilizofia Ulaya kutoka Uhundi zilikuwa ghali sana kwa sababu ya vituo vingi vya biashara kati ya Uhindi na Ulaya.

Kolumbus alitaka kufika Uhindi kwa meli bila kupita maeneo ya Waislamu upande wa mashariki. Alitaka kufanya majaribio: kama dunia ilikuwa kweli tufe ya mviringo -jinsi walivyofundisha wataalamu- ni lazima ya kwamba kuna njia kufika mashariki kwa kuelekea magharibi. Alijua taarifa ya msafiri Marco Polo aliyewahi kufika Uchina akaona bahari kubwa upande wa mashariki ya Uchina. Kolumbus aliamini ya kwamba bahari ile ingekuwa bahari ileile kama bahari ya Atlantiki inayoanza upande wa magharibi ya Ulaya. Hakutegemea ya kwamba angekuta nchi mpya kabisa kati ya Ulaya na Uhindi.

Nchi hii mpya ilikuwa bahati yake. Katika mipango yake alifanya kosa la kukadiria umbali kati ya Ulaya Asia kwa kiasi kidogo mno. Akiba za chakula na maji katika jahazi zake zisingetosha kufika Uchina. Kukuta nchi mpya njiani amabayo hakutegemea kulimwokoa.

Safari ya 1492[hariri | hariri chanzo]

Kolumbus aliondoka Hispania kwa jahazi tatu tar. 3 Agosti 1492. Tarehe 12 Oktoba 1492 alikanyaga mara ya kwanza eneo la Amerika katika kisiwa kimoja kisichojulikana ni kipi kwa hakika katika funguvisiwa ya Bahama. Akaendelea hadi Kuba na kisiwa cha Dominica akarudi Hispania mwaka 1493.

Alipofika kwenye visiwa vya Karibi katika Amerika ya Kati aliamini ya kwamba hivi vilikuwa visiwa vya kihindi. Akaviita "Uhindi wa Magharibi" na wakazi kwa lugha ya Kihispania "Indio" yaani Wahindi. Hadi kifo chake hakutaka kukubali ya kwamba nchi hii haikuwa Uhindi wala sehemu yoyote ya Asia lakini kitu kipya.

Safari za baadaye[hariri | hariri chanzo]

Kwa jumla Kolumbus alifanya safari nne hadi Amerika. Mwaka 1498 katika safari yake ya tatu alifika mara ya kwanza kwenye bara lenyewe katika mdomo wa mto Orinoco katika Venezuela. Kwa jumla alipoteza jahazi 9 katika safari zake.

Ramani ya safari nne za Kolumbus